Msumbiji: Mgogoro wa Kisiasa Katika Jimbo la Kati la Beira

Barua hii ya wazi imekuja baada ya uongozi wa chama cha Mozambican Resistance Movement (Renamo) kutangaza tarehe 28 Agosti kwamba Davis Simango, Meya wa mji wa Beira, hatosimama kugombea kiti hicho kwa muhula wa pili wakati wa uchaguzi utakaofanyika tarehe 19 Novemba 2009.

Kama majibu ya haraka kwa tangazo hilo, wafuasi wa Renamo na Simango waliojawa na hasira waliushikilia ujumbe wa chama ili kupinga uamuzi ya Alphonso Dhlakama wa kumtoa Simango na kumuweka Manuel Pereira. Uamuzi huo uliwasha cheche za maandamano ya siku mbili huko Beira, wakati watu wanaomuunga mkono Simango walipovamia mitaa na kudai uamuzi huo ubadilishwe.

Usiku wa ijumaa iliyofuatia, askari polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za mpira dhidi ya umati ambao ulikuwa umekusanyika mbele ya ofisi za Renamo katika maeneo ya Munhava. Wakati wa ghasia, ripota kutoka gazeti la kila siku la Beira, “Diario de Mocambique”, Antonio Chimundo, alivamiwa na wanachama wa Renamo ambao walimshutumu kuwa alikuwa akifanya kazi kwa ajili ya chama tawala cha Frelimo.

Wachunguzi wengi wa mambo wakiwemo wabunge wa Renamo wanaulaumu uamuzi wa Dhlakama na kumsifu Davis Simango kwa uamuzi wake wa kusimama kama mgombea huru. Nakala mama ya barua iliyo hapa chini inapatikana katika blogu yangu ya lugha ya Kireno.

Mheshimiwa, nisingeiacha fursa ya kuanika maoni yangu juu yako kama kiongozi wa chama ambacho wakati fulani kilikuwa ni chama kikuu. Kadhalika ningependa kukuahidi kuwa sitakusahau mwaka ujao wakati wa uchaguzi mkuu.

Naam, Sitasahau wakati nikikumbuka wengi ambao uliwaua kisiasa. Gazeti huru limechapisha orodha fupi ya maswahiba wako wa zamani ambao walipigana pamoja nawe katika Renamo. Lakini kwa uamuzi wako, walifukuzwa kwa madai ya “utashi” wa “kambi” (wanachama na waunga mkono).

Kwa sasa ni muhimu kusisitiza kuwa Bwana raisi wa Renamo haamui na hakuwahi kuamua kwa mujibu wa matakwa ya makambi; vivyo hivyo ulifanya kuhusiana na vita kali ambayo kwa majivuno unadai uliviamuru.
Bwana Dhlakama, kisiasa uliwaua wengi wenye uwezo mkubwa wa kuongoza vyombo vya siasa kuliko wewe, watu ambao, kwa uzito wa usomi wao, ustadi wa kidiplomasia na werevu, waliliinua juu jina la Renamo wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe,wakati wa mazungumzo ya amani, msamaha wa kitaifa na wakati wa mijadala ya Bunge. Leo hii, watu wa namna hiyo ni wachache mno katika historia nzima ya Renamo!
Mheshimiwa, siku hizi, wewe ni mwili uliokufa kisiasa. Msumbiji ni moja ya nchi chache duniani ambako “maiti za kisiasa” zinaishi bega kwa bega na walio hai, bila kuamsha kihoro kwa walio hai.
Naam, sitakusahau, baada ya kukubali masumbwi matatu ya kushindwa katika chaguzi tatu za Urais; sitakusahau, nimechoka kusikiliza uwongo wako usio na matokeo.
Mpendwa Bwana Rais wa Renamo, lazima uwe ni mmoja wanasiasa wanaodanganya sana katika nchi hii, na wanasiasa ambao huongea bila kuzingatia matokeo: ulitangaza kwamba usingeshiriki katika baraza la jimbo baada ya uchaguzi wa 2004. Lakini sasa bado upo umejaa tele, kimya; hukutaka kutambua matokeo ya uchaguzi wa 1999, lakini ulitambua; unadai kuwa wewe ni mwana demokrasia, lakini sote tunajua njia ambayo ulijaribu kumuua Davis Simango… maneno mengi ya nini?
Bwana Rais wa Renamo, hufai kujifananisha na kanga, bali na kuku mdanganyifu asiyechoka kutotoa mayai aliyoyataga. Katika nchi yangu, kuku wa namna hivyo huunguzwa midomo yao, kwa kuwa ukubwa wa midomo yao ni sawa na mayai wanayoyavunja.

Kama alivyosema Salamao Moyana, Wewe, Bwana Rais wa Renamo, ni mmoja wa wachache waliongiliwa katika Renamo ambao, pamoja na kugundulika, bado wanang'ang'ania kubaki. Na kwa kweli, Nasubiri habari zaidi 2009 baada ya kushindwa kwako vikuu na Amando Guebuza. Bora lililobakia kufanywa nawe ni kukaa kimya mpaka wakati wa uchaguzi. Baada ya kushindwa, itisha mkutano wa kutangaza ugombea wako kwa ajili ya uchaguzi wa 2014! Kisha, washirika wako watakuja kutoka Meringue (Wapambe wabebao silaha wa Dhlakama). Kwa sababu wale ambao wanakuunga mkono hivi sasa watafukuzwa na wewe mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka ujao, wakati utakapoanza kuamua ni nani atakayekuwakilisha Bungeni.
Ni vizuri ujue kuwa Beira hawakuungi mkono tena. Endelea kupokea mshahara bila ya kufanya kazi. Kwa sababu kufanya upinzani kwako ni kukaa na kivuli chako na kuanzisha fitna dhidi ya wale unaodhania wako tayari kuhudumia wananchi. Maisha marefu Bwana Rais! Iweke akilini kuwa 2014, watu kama hawa ambao wanakuunga mkono sasa watakuwa adimu.

1 maoni

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.