Colombia: Watu Wanaswa na Mitego ya Upatu

Hook, Line, Sinker na ToastyKen kuhusu blogu, Kwa kupitia picha za video na mtandao wa marafiki wa Facebook, raia wa Colombia, Diego Alejandro, anaweka wazi udanganyifu na utapeli mkubwa uliojificha nyuma ya michezo ya upatu ambayo inatangazwa kama njia mbadala za uwekezaji. Katika nchi ambapo akaunti za benki zimepoteza maana kwa sababu ada za uendeshaji ziko juu kuliko riba anayopata mwenye akaunti, michezo hii ya upatu inayoshawishi kumjaza mtu mapesa, ambapo raia wanalipa kiasi fulani cha pesa ili kujiunga na kisha kuingiza marafiki zao 7 kabla wao hawajaanza kufurahia riba ya juu ajabu (kati ya asilimia 40 mpaka 70) basi imekuwa ni kivutio kikubwa mno. Hivi sasa idadi ya wale wanaoingizwa mkenge na michezo hii inazidi kukua huku serikali ikijaribu kuweka mikakati ya kuwaadhibu wale wanaotumia umbumbu wa raia ili kuwakamua pesa kwa njia hizi za kidanganyifu.

DiegoAlejandro1985 ametuma picha ya video inayoonyesha watu wakiwa katika mstari wa kuingia katika moja ya taasisi zinazoendesha michezo hiyo inayojulikana kama DRFE wakijaribu kudai pesa zao mara baada Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuivamia na kuipekua, ambapo kuna fedha zilizokutwa zilizodhaniwa kuwa ilikuwa zitumike kulipa wale waliowekeza pesa zao kwenye taasisi hiyo, hata hivyo, msako huu unasemekana kwamba ulikuwa batili na hivyo mchezo wa upatu katika jengo hilo bado unaendelea.

Kupitia blogu yake, Denuncias y Más, Diego Alejandro anaeleza anayoyaona kwa kuwa amekuwa akifuatilia yale yanayoendelea katika michezo mbalimbali ya upatu inayoendeshwa nchini humo.

Kwa namna ya pekee iliyonihuzunisha na itakayowahuzunisha watapeliwa wa baadaye, DRFE ilinusurika kidogo kutokana na ufa ulio katika mfumo wetu “makini” wa haki; ofisi yao ilivamiwa na kupekuliwa na maafisa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na fedha ambazo zingetosha kuwalipa wahanga wa mchezo huu wa upatu uliokuwa umekwishafikia kikomo zilipatikana. Lakini katika hali isiyo ya kushangaza nchini Colombia, jaji aliyesikiliza shauri hilo alitangaza kwamba upekuzi huo hakuwa halali. Msako uliendeshwa baada ya kusambaratika kwa michezo mitatu ya upatu huko Pitalito Huila [Mhariri: hili ni jiji mojawapo huko kusini mwa Colombia].

Jukwaa la mjadala lijulikanalo kama The Laneros (ambalo ni jukuwaa la teknolojia nchini Colombia na ambalo hivi sasa limechukua sura ya kimataifa) linasema kwamba watu wamegawanyika kuhusu michezo hii inayotia shaka. Kundi la DMG, ambalo ni la wateja wa michezo hii wanatetea mfumo huo wakisema kwamba ni sawa kununua bidhaa bidhaa kwa mkopo na kisha kulipa polepole hata kama gharama inakuwa mara mbili ya thamani halisi ya bidhaa hizo, wanadai kwamba wao imewahi kuwasaidia, na kwamba hawakuwaki kupata matatizo yoyote ya kuzipata tena fedha zao, wakiamini kwamba biashara ndogondogo inayofanywa ndiyo hasa inayorudisha pesa zao; wakati huo huo wapo wanaotoa hoja kwamba pesa hizo hajizai au kuongezeka kwa namna yoyote, bali kile kinachoitwa kuwa gawio ni pesa za watu wanaoanza kuweka pesa zao kwenye michezo hiyo ili kuwekeza.

Mnamo mwezi wa Juni uliopita, polisi waliichunguza DMG na hivyo kusababisha wafunge shughuli zao kwa muda. DMG ina mtandao wake yenyewe wa YouTube unarushwa kwa lugha ya Kispanyora, na rais wake, David Murcia Guzmán, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akilaani vitendo vya serikali akidai kuwa ni vya unyanyasaji, papo hapo alidai kuwa haki itendeke katika kuendesha upelelezi na michakato ya kisheria kabla ya kuwahukumu wao kama matapeli, alitoa changamoto kwa serikali iliyo madarakani kuzingatia kwamba kuna ajira za moja kwa moja au zilizo kwa njia nyingine ambazo zinahusiana na shughuli za kampuni ya DMG. Unaweza kutazama video hizo kwa kubofya Sehemu ya 1 na Sehemu ya 2, moja baada ya nyingine. Ifuatayo ni upigaji picha uliofanywa wakati wa maandamano ya DMG:

Kama inavyoweza kuonekana katika mifano iliyo kwenye picha hizo, raia wengi wa Colombia hawaoenekani kuhusisha mbinu za DMG na michezo mingine ya upatu kwa sababu tu ili kujiunga nayo hawahitajiki kutafuta watu wengine wa kujiunga, na kwa hiyo wanaomwunga mkono David Murcia Guzmán ni wengi tu. Mfano mzuri unaweza kupatikana katika ukurasa wa marafiki wa Facebook: kundi la watu wanaopinga michezo ya upatu lina wanachama 35 tu, wakati kundi la “Marafiki wa David Murcia Guzmán” lina zaidi ya wanachama sitini elfu, na vilevile kuna makundi
mengine 12 ambayo yanahusiana kwa namna moja au nyingine na wanaounga mkono DMG.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.