Waziri matatani kwa cheti ‘feki’

Ali Kordan,Waziri wa Mambo ya Ndani wa Irani, Katika siku za hivi karibuni, ameshutumiwa vikali kwa kuonyesha Shahada ‘feki’ ya Udaktari (PhD) aliyodai kupata kutoka katika chuo kikuu chenye sifa kubwa duniani cha Oxford cha nchini Uingereza. Tovuti mbalimbali, pamoja na ile ya kihafidhina wa Alef, zimechapisha picha ya cheti hicho ‘feki’ cha Kordan kinachoonyesha kwamba ametunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima na Chuo Kikuu cha Oxford.

Alef inaonyesha makosa kadhaa ya kiuandishi yaliyojitokeza kwenye cheti hicho kinachodaiwa kuwa cha Oxford, kwa mfano, “to be benefitted from its scientific privileges”. Pia neno“entitled” liliandikwa kimakosa “intitled”.

Vilevile tovuti ya Alef imepandisha kwenye ukurasa wake faksi kadhaa ambazo iliandikiana na Chuo Kikuu cha Oxford kuhusiana na jambo hili. Baada ya hapo tovuti hiyo ilizuiwa kuonekana nchini Iran.

Wakati ambapo mamlaka nchini Irani inafanya upelelezi kuhusiana na jambo hili, Chuo Kikuu cha Oxford kimetangaza kwamba hakina kumbukumbu kwamba Bwana Kordan alipata kuhitimu katika chuo hicho.

Mwanablogu wa Irani, Bwana Behi, anaandika:

Rais Ahmadinejad amefanya muujiza mwingine. Amemteua mtu anayedai kuwa na Shahada ya Udaktari katika Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Oxford kama waziri wa mambo ya ndani! Yalipoibuliwa maswali kuhusu uhalisia wa shahada hiyo, huyo jamaa alijawa na jazba, alivitishia vyombo vya habari na kuonyesha cheti chake hiki. Cheti chenyewe kinatia mashaka makubwa na kinadhaniwa kuwa ni cha kughushi, tena kimejaa makosa ya kiuandishi na wakati huo huo majina yanayoonekana kwenye saini wala si ya yeyote miongoni mwa wanaofundisha katika Kitivo cha Sheria cha chuo hicho! Ikiwa Ahmadinejad anataka kughushi katika uchaguzi ujao, basi heri atafute mtu makini wa kumsaidia katika kugushi pasipo kugundulika kwa urahisi. Lo, aibu kubwa hii!

Mohmmad Ali Abtahi, aliyekuwa Makamu wa Rais katika serikali ya kimageuzi na ambaye pia ni mwanablogu, anaandika kwamba enzi zake alipokuwa Naibu Waziri wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu, aliwahi kukutana na afisa mmoja wa Irani ambaye aliwahi ‘kununua’ Shahada ‘feki’ ya Udaktari. Abtahi anasema kwamba bei ya kununua cheti kama hicho ilikuwa ni karibu dola za Marekani 1000.

Mwanablogu mwingine, Shirzad [Fa], anadai kwamba kuna uwezekano mkubwa kuwa Ali Kordan hana hata shahada ya kwanza. Mwanablogu huyu anaongeza:

Inamaanisha kwamba miaka yote hii waziri huyu ametumia udanganyifu kulipwa kama mtu mwenye Shahada ya Udaktari … Mmoja wa wasaidizi katika Bunge la Irani aliwahi kumuuliza Kordan: “Ulipataje Shahada yako ya Udaktari katika Sheria wakati wewe unadai kwamba uliandika Utafiti (Thesis) wako kuhusu Elimu ya Kiislamu?” “Je, ulifanya vipi utetezi wako wakati ambapo wewe huwezi kuzungumza Kiingereza?” Kordan alijibu, “Nilikuwa na mfasiri.”

Mwanablogu Jomhour anaandika kwamba [Fa] Rais wa Irani, Mahmoud Ahmadinejad alimtetea Waziri wake kwa kuuliza, “Je, ni nani aliye na haja na makaratasi haya yanayoweza kuchanwa (yasiyo na maana)!”

Mwanablogu huyu anauliza:

Endapo vyeti havina maana, ni makaratasi yanayoweza kuchanwa wakati wowote, hivi basi kwa nini Waziri wa Ahmadinejad alijihangaisha kutafuta walau cheti hicho feki … na hii si mara ya kwanza ambapo Rais Ahmadinejad anaita (anakebehi) nyaraka muhimu kuwa ni makaratasi yanayoweza kuchanwa wakati wowote kumaanisha kwamba hayana maana. Hapo mwanzo aliwahi kusema kuwa nyaraka zilizoonyesha msimamo wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Mpango wa Nyuklia wa Irani kama makaratasi yasiyo na maana.

Ali Akbar Javanfekr, Mshauri wa Rais Ahmadijad katika masuala ya mawasiliano na vyombo vya habari, anasema kwamba [Fa] Wizara ya Sayansi itoe uamuzi kuhusu Shahada ya Udaktari ya Kordan na anapendekeza kwamba tusiingize au kuhusisha katika siasa mtazamo na maoni binafsi kuhusu suala hili.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.