Karibeani: Radi ya Bolt Yaipiga Beijing


“Radi ya Bolt” – Picha na hybridvigour. Tembelea mtiririko wa picha zake.

Ujumbe huu utakuwa mrefu kama ufupi wa mtoko wa Mjamaika Usain Bolt kuelekea chaki ya ukomo wa mbio za mita 100 na utukufu wa Olimpiki ulivyokuwa mfupi na mtamu – kwa sababu mabloga wa Karibiani bado hawajashuka kutoka kilele cha furaha ambacho kimeumbwa na ushindi wa Bolt. 9.69 ndiyo iliyokuwa namba ya bahati iliyompatia dhahabu mkimbiaji wa Kijamaika. Sekunde 9.69. Na alifanya hivyo, Kwa mujibu wa nukuu katika gazeti la New York Times, ‘kwa maili.’

Kana kwamba utawala wa kimahiri wa Bolt kwenye medani ya “binadamu mwenye mbio kuliko wote” haukutosha, Mtrinidadi Richard Thompson ambayeye alionyesha mvuto mwanzoni mwa mwaka katika mashindano ya NCAA, aliposhinda dhahabu kwenye mita 100 na mita 60 (kwenye viwanja vya ndani) alichukua ushindi wa kushangaza kwa kuchukua nafasi ya pili.

Twita na Facebook mara moja vikaingia mtamboni, huku mabloga wakiziita “mbio za Olimpiki” na kukiri kuwa “wanajivunia kuliko kawaida kuwa Wahindi wa Magharibi”

Umuhimu wa Wakaribeani kushika nafasi ya kwanza na ya pili katika moja ya michuano mashuhuri ya michezo ya Olimpiki ulianza kuwaingia. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza tangu mashindano ya mwaka 1976 kule Motreal (wakati Mtrinidadi Hasley Crawford alipochukua heshima ya juu) kwa Muhindi wa Magharibi kuleta nyumbani dhahabu katika mbio za mita 100. Mafanikio mengine muhimu ni ukweli kwamba sita kati ya wanane waliofikia fainali hizo walikuwa wakitoka katika dola jirani. Kwa maneno ya bloga wa Kijamaika Active Voice:

Hivi sasa inaonekana kuwa Karibeani ndiyo inayotawala mashindano ya mbio!

… wakati West Indies Criket Blog anaongeza:

Wow! Ni Wow tu!

Inaeleweka kwa Wajamaika kuwa na majivuno haya! Anasema bloga, Blog to the World:

Ilikuwa patashika na chereko za kiwehu-wehu wakati Mjamaika Usain Bolt aliposhinda mbio za mita 100 katika Olimpiki katika rekodi ya sekunde 9.69 (alipojivunjia rekodi yake mwenyewe ya sekunde 9.72. kinachostaajabisha zaidi kuhusu namna alivyoshinda ni kuwa alianza kusherehekea kukiwa bado na mita 20 za kumalizia.

Kabla kutoka mlangoni kwenda kujiunga na msafara wa magari uliokuwa ukiendelea huko Falmouth”, naye pia anasema ushindi huu ulikuwa una maana maalum kwake pia, kwa vile anamfahamu Bolt kwa ukaribu:

Anatokea katika kitongoji cha Sherwood katika wilaya yangu ya Trelawny. Alipokuwa shule ya sekondari ya juu (Shule ya kumbukumbu ya William Knibb) karibu kila jioni alikuwa akibarizi kwenye duka langu la luninga kabla ya kwenda nyumbani kwa hiyo nimekuwa nikangalia maendeleo yake kwa miaka kadhaa.

Kabla ya ushindi, kuna mabloga wengine walikuwa wakitania kwamba “dawa kabambe” inayopelekea ushindi wa hali juu namna hii kutoka kwa Wajamaika ni ile Wahindi wa Magharibi wanayoiita “chakula cha buluu” – yaani vyakula kama magimbi na mizizi mingine mingine.

Bloga Montego Bay Day By Day anaafiki kwamba “magimbi ya njano, pamoja na nazi vinarutubisha mwili”, lakini hakufurahika kwa vile NBC hawakurusha matangazo moja kwa moja ya mbio hizo:

Je kama Tyson Gay angefaulu katika kinyang'anyiro cha kupata nafasi kwenye fainali wangefikiria umuhimu wa kurusha matangazo hayo, japokuwa Gay angechabangwa vizuri na Bolt? Simulizi ya “sizitaki mbichi hizi kwa kweli… Masikini Asafa powell hakupata hata shaba.. lakini ndiyo mambo yanavyokuwa mara nyingine. Haya peteni Wahindi wa Magharibi!! Mnatutia majivuno!!

Ama kwa hakika, jumbe za kujivunia zinazidi kumiminika. Mjamaika Stunner anauliza:

Iweje nisijiunge na wimbi la mabloga wajivunaji wanaopongeza uvunjaji wa rekodi uliofanywa kistadi na Usain bolt? Uvunjaji huo wa rekodi ulikuwa ni wa kustaajabisha lakini linalosisimua zaidi ni ukweli kwamba Bolt alipunguza kasi na kuanza kusherehekea ushindi wake takriban kwenye alama ya mita 80! Ama kweli! Unaweza kufikiria ingekuwaje kama asingepunguza kasi?

Mara tu kanda nzima (ya Karibeani) ikaanza kuchangia. Bloga wa Ki-Barbados aliye ughaibuni Jdid anasema:

Inakuwaje jina alilopewa linamstahili hivi huyu bwana? Bolt (mshale mfupi au radi kwa Kiswahili)! Sekunde 9.69 na alikuwa tayari anasherehekea alipofika mita 80. Hongera! Jivuneni Jamaika! Jana usiku kwenye CBC (Kanada) walikuwa na mjadala kuhusu kwa nini Jamaika imetengeneza wakimbiaji wa kasi wa mbio fupi kwa miaka mingi…

Bloga Moving Back To Jamaica inaonekana ana jawabu:

Kama kuna jambo ambalo sisi Wajamaika tunaweza kutarajiwa, ni kufurahia ukweli kwamba tunacho kiwanda cha kutengeneza wakimbiaji kasi duniani. Wasichokijua wengi ni kwamba sababu kubwa ya mafanikio yetu ni ushindani mkali uliopo kwenye mashule yetu ya sekondari, ushindani ambao huanzia katika umri wa miaka 11 na kudumu maisha yote.

Kuwepo kwa siri au la, hakuna shaka juu ya uwezo wa Bolt. Bloga Living in Barbados alimpachika jina mkimbiaji #1 duniani kama “silaha ya maangamizi”, wakati bloga wa visiwa vya Cayman Mad Bull alimuita “radi iliyopakwa mafuta”, na akaongeza:

Jambo moja tu ni kwamba, unaweza kufikiria ni muda gani angetumia kama angalikimbia kwa uwezo wake wote tangu mwanzo mpaka mwisho wa shindano?! Wow! Alifunga kazi na kuanza kusherehekea kuanzia takriban alipofika mita 75! Samahani, hakukaza nia mbio nzima, ili kwamba tujue lile ambalo ana uwezo wa kulifanya!

Media Watch aliyeko Trinidad na Tobago waliliita shindano lile “la kustaajabisha! Safi sana! lenye supaku za umeme!” kabla ya kuingia kwenye kuzikosoa huduma duni za vyombo vikuu vya habari katika kutangaza tukio hilo – pengine angekwenda kwenye mtandao, ambako bloga Andre Bagoo alikuwa akiblogu moja kwa moja shindano hilo.

Heko zilizidi kumiminika – kutoka Grenada, Guyana na Trinidad na Tobago.

Habari zikafika kwamba Waziri Mkuu wa Jamaika Bruce Golding ameahidi sherehe kubwa ya mapokezi kwa Mjamaika wa kwanza kutwaa medali ya dhahabu kwenye Olimpiki ya Beijing, Usain Bolt, pamoja na timu nzima ya Olimpiki, Bloga Living Guyana anapendekeza njia kadhaa za kumuenzi mwanaolimpiki huyu aliyetia fora:

Ikiwa… Bruce Golding… ana uwezo kidogo wa kufikiri angetoa tamko kuwa Jumatatu iwe sikukuu ya kitaifa nchini Jamaika, na angeubatiza mtaa wa Knutsford Boulevard, kama barabara kuu ya Usain bolt na angeamuru kuwa Agosti 16 ni siku ya Usain Bolt. Anapaswa kupewa ardhi, yenye ukubwa wa maili za mraba 9.69 nchini Jamaika. Na nyumba vile vile.

Lakini si wote waliopigwa butwaa na “Radi ya Bolt”. Wakati bloga Living Guyana alijibu swali la BBC kurasa ya michezo na mwanahabari Matt Slatter kwenye Twita lililouliza “Je, ni kweli nimemuona mwanadamu anayekimbia upande upande, akijipigapiga kifua na aliyeweza kukimbia mita 100 kwa sekunde 9.69? Alimjibu pia kwa namna ya uhakika “Ah ni kweli Matt umemuona. Macho yako hayakukudanganya”. Mjamaika Long Bench alidhani majigambo yalizidi kidogo:

Natumaini kuna mtu atamkumbusha kuwa yeye bado ni mwanadamu. Watu wenye kujidai huwa wanavumiliwa kwa mda fulani tu, hata kama ni Wajamaika, na hata wangekimbia kasi namna gani.

Katikati ya kufurahia ushindi wa wazalendo wenzake kutoka Karibeani, Living Guyana alijisikia kuwasononekea kundi la Olimpiki kutoka Guyana:

Nchi mbili za Karibeani zilizowekeza vikubwa kwenye riadha zinaona matunda yake na zinafurahia kutambulika kwenye ulingo wa dunia. Nchi hizi mbili zina viwanja vinavyofaa kwa riadha, programu nzuri za riadha, wakufunzi wazuri… na katika habari nyingine wanariadha wa Guyana wanaendelea kutolewa kwenye michuano ya Olimpiki hata bila ya kutambulika.

Hata hivyo, hakuna lililoweza kupunguza wimbi la furaha lililofunika Uhindi Magharibi wakati visiwa viwili vilivyoko kwenye ncha mbili tofauti za visiwa hivyo vilileta nyumbani dhahabu na fedha kutoka katika michuano ya juu ya Olimpiki ya 2008. Habari njema zimeenea kuanzia Uchina mpaka Karibeani, kutokea fukwe za visiwa mpaka ughaibuni na kila mahala. A Mi Ver, aishiye Florida, alikamata namna ya majivuno na mafanikio wakati aliporejea mazungumzo na baba yake, ambaye alimpigia simu kutokea Trinidad kumfahamisha yaliyojiri:

“Nimeamua kuvunja sheria leo hii kwa sababu tunasherehekea” mzee alisema, “ninakupigia wakati nikiendesha barabarani. Usain Bolt wa jamaika ameshinda dhahabu kwenye michuano ya mita 100 ya wanaume, Richard Thompson wa Trinidad amenyakua fedha na Marekani wameambulia ushindi wa tatu.”
Anasikika mwenye furaha akipiga simu hivi.
*Dakika tano baadaye*
“Aye” anasema mzee. “Hivi nimeshakueleza kuwa watu wawili kutoka Karibeani ndiyo wana kasi kuliko wote duniani?”
“Naam, nafikiri ulishaniambia.”
“Sawa nakwenda.”
“Sawa. Kwa kheri, Baba. Nakupenda, Endesha salama.”
“Nakupenda pia. Mwanangu. Tumeshinda, eh!”

1 maoni

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.